KUJAA MAJI KWENYEGOTI/KNEEL EFFUSION.

Maji Kwenye Goti Ni Tatizo Gani?

Maji kwenye goti (knee effusion au water on the knee) ni hali ya kupata maumivu makali kutokana na maji kujaa kuzunguka au ndani ya maungio ya mifupa ya kwenye goti (knee joint). Hali hii ikitokea, kujua chanzo na dalili zake na njia bora ya kuyaondoa maji hayo kwenye goti ni kitu muhimu. Njia utakayoitumia kuuondoa uvimbe huu itategemea chanzo cha uvimbe na daktari anaweza kuhitajika kufanya uchunguzi.

Kiasi kidogo cha maji huwepo kwenye joint ya kawaida. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 27 ya watu hupata tatizo la maji kwenye magoti kwa muda fulani.

Umbile  La Goti

 

Goti ni jointi iliyo kubwa na yenye sehemu nyingi kuliko jointi zote katika mwili. Jointi ya goti huunganisha mfupa wa paja (femur) na mfupa wa chini ya goti (tibia). Mfupa mdogo unaokwenda sambamba na mfupa wa chini ya goti (fibula) na kifuu cha goti (patella) ni mifupa mingine inayojenga jointi ya goti. Tendoni huiunganisha mifupa ya goti na misuli ya miguu ambayo huchezesha jointi ya goti. Ligamenti huiunganisha mifupa ya goti na kulifanya goti kuwa na utengamano.

. anterior cruciate ligament hufanya kazi ya kuzuia mfupa wa femur kuzunguka nyuma kwenda kwenye tibia (au tibia kuzunguka mbele kwenda kwenda kwenye femur.)

. posterior cruciate ligament huzuia femur kuzunguka mbele kuja kwenye tibia (au tibia kuzunguka nyuma kwenye femur.)

. medial na lateral collateral ligaments huzuia femur kwenda upande. Vipande viwili vya gegedu (cartilage) vyenye umbo la C viitwavyo medial na lateral menisci hufanya kazi ya shokomzoba kati ya femur na tibia.

Vifuko vidogo vilivyojaa maji (bursae) hufanya kazi ya kulilainisha goti.

 

Dalili Za Maji Kujaa Kwenye Goti

 

Bila kujali ni nini chanzo cha maj kwenye goti lako, dalili huwa zinafanana. Ukali wa dalili hutofautiana kutoka mtu hadi mwingine. Dalili za kawaida za kuwa na maji kwenye goti ni kama zifuatazo:

Kuvimba: Uvimbe mdogo au hadi uvimbe mkubwa

Maumivu: kupwita kwa kawaida hadi maumivu makali ya kuchoma yanayozuia mwondoko

. Kukakamaa: kupunguza umbali wa kukunjuka wa jointi au kuzuia kabisa mwondoko

Wekundu na joto: kunakoambatana na uvimbe.

Kutegemeana na chanzo cha tatizo lako la kujaa maji ndani ya goti, unaweza kuona dalili nyingine kama zifuatazo:

. Kuchubuka au kuvuja damu kwenye eneo la jointi (kutokana na kuumia)

. Homa, kutetemeka, na udhaifu (kama kuna maambukizo)

. Kupungua kwa misuli (kutokana na arthritis sugu, kunakoitwa arthrogenic muscle inhibition)

Hali mbaya inayotokana na uwepo wa maji ndani ya jointi ni kujijenga kwa kivimbe kilichojaa maji, kiitwacho Baker’s cyst, ndani ya eneo la jointi. Kivimbe hiki hutokea pale maji yanapokuwa mengi kiasi cha kushindwa kufyonzwa na mwili. Kivimbe cha Baker’s cyst kikiwa kidogo hakina dalili zo zote, lakini vivimbe vikubwa unaweza kuvitaambua kwa kuvigusa na huleata maumivu wakati wa kutembea.

 

Uchunguzi

 

Uchunguzi wa maji kwenye goti unaweza kuhusisha kukitazama kiungo husika, imaging tests, na vipimo vya maabara vya maji ya kwenye jointi yako. Kwa nyongeza, daktari atapitia historia yako ya kiafya, afya yako ya sasa hivi, na dalili anazoziona.

Ukaguzi Wa Mwili

Daktari wako atakagua jointi yako kwa kiundani. Atagusa (papasa) na kukunja jointi, na akajua mamo mengi kuhusu chanzo cha kujaa maji kwenye goti lako. Kwa mfano:

. Ikiwa ni arthritis, tishu ya kulainisha katikati ya jointi, iitwayo synovium, itakuwa laini, ya urojorojo. Isipokuwa wa gout, uvimbe wa aina nyingi za arthritis utakua taratibu na si ghafla.

. Maambukizo kwenye jointi hulata uvimbe ghafla na huwa na maumivu makali na wekundu kwenye jointi.

. Uvimbe wa ghafla unaoambatana na kutoweza kuhimili uzito unaashiria kuchanika kwa ligamenti au kuvunjika kwenye goti.

Imaging Tests

Baada ya kukagua jointi yako daktari anaweza kuagiza vipimo vya picha ili kukijua kwa uhakika chanzo cha maji kwenye goti lako. Kila kipimo kina ubora wake na mapungufu yake. Vipimo hivi vyaweza kuwa:

. Ultrasonography

. X-rays ba computed tomography (CT)

. Magnetic resonance imaging (MRI)

Ultrasonography inatumia mawimbi ya sauti kukagua mifupa na tishu zinazounganisha jointi. Inaweza kubaini arthritis na uvimbe wa tendoni au ligamenti. Kikiwa na faida ya kutoharibu tishu na kuhamishika, kikpimo hiki hakiwezi kuona tishu laini kama vipimo vingine vya picha

. X-rays and computed tomography (CT), vyote vikitumia mionzi, ni bora zaidi katika kuchunguza kuvunjika kwa mifupa na arthritis

. Magnetic resonance imaging (MRI),hutumia mawimbi ya sumaku na radio (magntic fields and radio waves). MRI hutumika kuchunguza tishu laini, gegedu (cartilage), na maumbile ya jointi vitu ambavyo havionekani kwenye vipimo vingine.

Uchunguzi Wa Ute Ute

Daktari anaweza kuagiza kutolewa maji (aspirate) kwenye goti lililovimba. Hii itasaidia kupunguza msukumo na kuondoa maumivu kidogo. Ute ute huu uitwao synovial fluid, huondolewa kwa utaratibu uitwao arthrocentesis. Daktari atautazama ute ute huo, na anaweza kuagiza upelekwe maabara kwa uchunguzi.

Ute ute kwa kawaida hauna rangi na una unato unaofanana na ule wa sehemu nyeupe ya yai. Mabadiliko yo yote ya mwonekano, muundo na seli zinazoujenga vinaweza kutoa dokezo juu ya sababu ya kutokea kwa maji hayo kwenye goti.

Endapo maambukizo yatahisiwa, maabara inaweza kufanya culture ili kuotesha na kutenganisha bakteria au fungus walioshambulia.

Sababu Za Magoti Kujaa maji

 

Kuvimba kwa goti kunaweza kusababishwa na kuumia, arthritis, matumizi ya kupitiliza ya goti, cysts au maambukizo ya vidudu. Maji ya kwenye magoti yanaweza kukufanya ukose raha na mara nyingi ni ishara ya tatizo kwenye goti. Aina ya maji yanayojaa kwenye goti itategemea aina ya ugonjwa, hali iliyofikiwa, au aina ya ajali iliyosababisha maji hayo. Daktari anaweza  kuchukua sampuli ya maji hayo ili yakapimwe kwenye maabara. Majibu yataeleza chanzo na tiba inayotakiwa kutolewa.

Majibu yanaweza kuonyesha uwepo au kutokea kwa moja ya yafuatayo:

. kuumia, kulikosababisha kuvunjika au kuharibu ligamenti.

. rheumatoid arthritis

. osteoarthritis

. gout

. pseudogout

. septic arthritis

. tuberculosis arthritis

. juvenile rheumatoid arthritis

. matumizi makubwa ya joint, kama michezo na shughuli nyingine za mwili

. maambukizo ya vidudu, kama Lyme disease au sphylis

. reactive arthritis

. inflammatory bowel disease

. hemarthrosis, au kuvuja damu ndani ya joint.

 

Uzito mkubwa au unene wa kupindukia unaweza kuongeza uwezekano wa kuumiza jointi ya goti.

Maji kwenye goti ni dalili ya kuwepo kwa uvimbe (inflammation), na tatizo hilo linaweza kugawanywa katika makundi makubwa mawili ya uvimbe uliotokana na maambukizi (septic) au uvimbe ambao haukutokana na maambukizi (aseptic).  Tatizo la maji kwenye goti linalotokana na maambukizi huitwa “septic arthritis”. Maji kujaa kwenye goti kusikotokana na maambukizi hutokana na kuumia au arthritis.

Maambukizi

Septic arthritis,  mara nyingi hutokana na mambukizi ndani ya jointi. Maambukizi yanaweza kutokana na kidonda, kama kuumia kwa ndani ya wakati wa tiba. Maambukizi ndani ya mfumo wa damu-yanayoitwa systemic infection-huweza kuishia kwenye jointi na kusababisha kuvimba na maji ya ziada.

Kuvimba goti kunakosababishwa na maambukizi huleta dalili za haraka sana. Maji ndani ya goti yaliyosababishwa na maambukizi kwenye huleta maumivu makali, na hasa wakati wa kutembea. Kuna mazingira yanaweza kuongeza yamkini ya kupata septic arthritis, nayo ni:

. Umri mkubwa

. Kisukari

. Matumizi ya madawa ya IV

. Kubadilishiwa jointi

. Upasuaji wa karibuni kwenye jointi

. Arthritis

. Kupungua kwa kinga za mwili (kama vile hatua ya mbali ya UKIMWI, wagonjwa walio kwenye tiba ya chemotherapy.)

Kuumia

Kuumia kwenye michezo ni sababu ya kawaida ya kuwa na maji kwenye jointi, na hasa goti- kama kupata ajali ya gari, kuanguka vibaya -vinaweza kusababisha magoti kujaa maji. Kuumia kunaweza kuhusisha mifupa, tishu za kuunganisha (kama tendoni au ligamenti), au gegedu (cartilage) ya kwenye jointi.

Misukosuko ya mara kwa mara kwenye jointi inaweza kusababisha kujaa kwa maji. Kuumia kwa aina hii hutokea pale kunapokuwa na kujirudia rudia kwa mwondoko, na mara huendana na shughuli ya kikazi au mchezo. Watu wapatao tatizo la maji kwenye jointi kutokana na kujirudiarudia kwa misukosuko, mara nyingi bursitis ((the inflammation of the fluid-filled sac that cushions a joint) na tenosynovitis (inflammation of the tendon sheath where a muscle attaches to a bone) huwa ndiyo sababu.

Maumivu, uvimbe na shida kunyoosha au kuzungusha jointi ni dalili za kawaida za kuvimba kwa goti kutokana na kuumia.

Arthritis

Kwa wagonjwa wa arthritis, kujaa maji na kuvimba kwa jointi ni vitu vya kawaida. Arthritis inaweza kuwa sugu (chronic) au kuleta vipindi vya uvimbe wa ghafla (acute), ambao unaweza kuleta kujaa kwa maji.

Kiujumla, kuna aina mbili za arthritis:

. Osteoarthritis, ambako ni kuchoka “wear-and-tear” kwa jointi.

. Autoimmune arthritis, kama vile rheumatoid arthritis, gout, juvenile idiopathic arthritis, ambako mfumo wa kinga za mwili hushambulia tishu za jointi.

Maji kujaa kwenye jointi kutokana na osteoarhtritis huonekana zaidi kwenye magoti na huambatana na uharibifu mkubwa wa jointi. Maji kujaa kwenye jointi kunakotokana na autoimmune arthritis huambatana na uvimbe wa muda mrefu au wa ghafla.

Ni kawaida kupata tatizo hili kutokana na gout, ambao ni ugonjwa wa kinga za mwili unasbabaisha kujaa kwa crystali za uric acid kwenye eneo la jointi (hasa dole gumba la mguu). Dalili za gout zinaweza kuwa nzito na hutokea ghafla, ba huweza kasababisha maji kwenye eneo linalozunguka jointi.

 

Tiba Ya Maji Kwenye Goti

 

Tiba ya kwanza kabisa inayoshauriwa ya maji kwenye goti ni pamoja na kupumzika, kuweka barafu, kutotembea, na kutumia non-steroidal anti-inflammatory drug (NSAID) kama Advil (ibuprofen) au ASleve (naproxen).

Kama uvimbe wako ni mkubwa sana, daktari anaweza kunyonya maji kama sehemu ya tiba. Unaweza kudungwa sindano ya cortisone baada ya kumyonywa maji. Hii inaweza kukupunguzia maumivu na uvimbe haraka, hasa kama kuna kidonda kikubwa au uharibifu mkubwa kutokana na arthritis.

Maambukizo yanaweza kutibiwa kwa kutumia dozi ya siku 14 ya broad-spectrum antibiotics za kunywa kama vile ciprofloxacin. Hali mbaya zaidi, kama zile zinazopokana na systemic gonorrhea au methicilin-resistant Staphylococcus aureus (MRSA), zinaweza kuhitaji kati ya wiki mbili hadi 4 za antibiotics za kwenye mishipa.

Kama una rheumatoid arthritis au namna nyingine ya autoimmune arthritis, hatua zinaweza kuchukuliwa kuidhibiti hali yako. Hii ni pamoja na kutumia immune-suppressive drugs, kama methotrexate na Humira (adalimumab), zinazolenga kupunguza kasi ya utendaji wa kinga za mwili.

Arthroplasty (joint surgery) hutumika kama kuna kuumia vibaya sana kwa jointi au jointi kushindwa kufanya kazi kwa sababu ya arthritis. Hali mabaya zaidi zinaweza kuhitaji kubadilishiwa jointi.

 

Katika mada yetu nyingine tutauzungumzia kwa kina ugonjwa wa rheumatoid arthritis. Usisite kutoa maoni yako kuhusu uandishi wa mada yetu ya leo.

Comments

Popular posts from this blog

𝗦𝗘𝗛𝗘𝗠𝗨 𝗞𝗨𝗨 𝗠𝗕𝗜𝗟𝗜 𝗭𝗔 𝗠𝗙𝗨𝗠𝗢 𝗪𝗔 𝗨𝗭𝗔𝗭𝗜 𝗞𝗪𝗔 𝗠𝗪𝗔𝗡𝗔𝗨𝗠𝗘 (𝗧𝗪𝗢 𝗠𝗔𝗜𝗡 𝗣𝗔𝗥𝗧𝗦 𝗢𝗙 𝗠𝗔𝗟𝗘 𝗥𝗘𝗣𝗥𝗢𝗗𝗨𝗖𝗧𝗜𝗩𝗘 𝗦𝗬𝗦𝗧𝗘𝗠)

TIBA YA MAUMIVU YA MAUNGIO

What are Kidney Stones?